MARUFUKU KUKATA PESA ZA WAKULIMA

DENDEGO

 

SERIKALI mkoani Mtwara imepiga marufuku kwa vyama vya msingi na mabaraza ya madiwani mkoani hapa kuweka utaratibu wa kukata pesa kutoka katika malipo ya tatu ya mauzo ya korosho wanazotarajiwa kulipwa wakulima hao baadae mwezi huu.

Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa mkoa wa Mtwara. Halima Dendego alipokuwa akijibu swali la Halfan Makota mkulima wa kijiji cha Makong’onda kata ya Mnavila wilayani Masasi aliyetaka kujua juu ya kuwapo kwa mpango wa halmashauri ya wilaya yao kuwakata shilingi 20 katika kila kilo ya korosho walizouza watakapolipwa malipo yao ya tatu.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa ni marufuku kumkata mkulima hata senti moja kwani tayari makato kwaajili ya kuchangia shughuli za maendeleo kutoka katika malipo yao ya awali waliokwisha kulipwa hivyo hakuna haja ya kuleta michango mipya.

“Ndugu zangu nataka niseme hapa kwamba kuanzia leo ni marufuku kwa baraza la madiwani au chama cha msingi kukata fedha za wakulima kutoka katika malipo yao ya tatu…kwani jamani hawa si walishakwishakuchangia kwa kukatwa katika malipo yao ya awali sasa nini tena ebu tuwaache fedha hizo wazitumie kwa kugharimia elimu ya watoto wao”, alisema Dendego.

Awali mkuu huyo wa mkoa ambaye alikuwa katika siku yake ya pili ya ziara ya kutembelea wilaya hiyo mara baada ya kukagua ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari ya kata ya Mnavila, alitoa nafasi kwa wanakijiji kumuuliza sawali kama walikuwanayo.

Baada ya kupata nafasi hiyo ndipo mkulima huyo alipotaka kujua juu ya kuwapo kwa fununu kuwa halmashauri ya wilaya hiyo imepanga kuwakata shilingi 20 kwa kila kilo ya korosho na kama mpango huo upo umeridhiwa na nani na kwanini wao kama wakulima hawakushirikishwa.

Kabla ya kujibu swali hilo mkuu huyo wa mkoa alimuinua diwani wa kata hiyo Meja mstaafu wa jwtz. Ramadhani Chilumba, kutoa maelezo kama jambo hilo lipo na lilipitishwa na baraza la madiwani.

Diwani huyo alikili kuwapo kwa hoja ya kutaka wakulima wakatwe kiasi hicho cha fedha ili kuchangia ujenzi wa maabara lakini suala hilo baada ya kujadiliwa kwa kina halikupitishwa na kwahiyo halipo.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa hili jambo ni kweli lililetwa na mjumbe mmoja na likapata nafasi ya kujadiliwa na mimi ndio nilikuwa wa kwanza kuchangia hoja hiyo na nilikataa kabisa na waliofuata waliniunga mkono na baraza likakubaliana fedha hizo zitafutwe kwa namna nyingine na sio kuwakata wakulima”, alisema Chilumba.

Baada ya majibu hayo ndipo mkuu huyo wa mkoa alipotoa kauli ya serikali kwamba ni marufuku kumkata mkulima kutoka katika malipo yake ya tatu ya mauzo ya korosho msimu huu ambazo wanatarajiwa kulipwa hivi karibuni.

Chini ya mfumo wa ununuzi wa korosho wa mfumo wa stakabadhi gharalani mkulima anapewa malipo ya kwanza baada ya kukusanya korosho zake katika chama cha msingi na analipwa malipo ya pili baada ya kuuzwa na malipo ya tatu huwa ni baada msimu kufungwa na kukokotoa hesabu za biashara baada ya kutoa gharama za uendeshaji ndipo mkulima anapata malipo ya tatu.

Mwisho.

 

Advertisements